VPL: Mechi 7, Simba kuendelea kubaki kileleni au kuwapisha Stand United wikendi hii…

Nahodha wa Stand United Jacob Masawe (kulia) akimzuia Ajib

MECHI 7 za ligi kuu Tanzania Bara zinataraji kuchezwa mwishoni mwa wiki hii. Siku ya Jumamosi kutakuwa na game tano.
Vinara wa ligi hiyo, Simba SC wataikaribisha Kagera Sugar FC katika uwanja wa Uhuru. Huko, Turiani, Morogoro wenyeji Mtibwa Sugar FC watakuwa na kibarua kigumu mbele ya Tanzania Prisons.
JKT Ruvu ya Pwani baada ya kubanwa mbavu na Prisons siku ya Jumatano, kesho watawaalika timu ya Mwadui FC katika uwanja wa Mabatini, Mlandizi.
Baada ya kuwachapa Azam FC katikati ya wiki, Stand United wataendelea kubaki nyumbani, Kambarage Stadium, Shinyanga kuwavaa African Lyon.
Mechi ya mwisho siku ya Jumamosi itapigwa katika uwanja wa Kirumba, Mwanza wakati wenyeji Toto Africans itakapowakaribisha vibonde wa ligi hiyo Majimaji FC ya Songea.
‘Mechi ya wiki’ itapigwa siku ya Jumapili wakati makamu bingwa mtetezi Azam FC itakapokuwa wenyeji wa mabingwa watetezi Yanga SC katika dimba la Uhuru.
Ruvu Shooting itakuwa nyumbani Mabatini kucheza na Mbeya City FC.
SIMBA v KAGERA
Kocha, Mecky Maxime bado anawekeza mbinu zake katika kikosi cha Kagera. Anakutana na Simba isiyopoteza mchezo wowote hadi sasa.
Simba imefanikiwa kufunga jumla ya magoli 15 na kuruhusu magoli matatu katika mechi 8 walizocheza. Pointi 20 zimewaweka juu ya msimamo na hawajapoteza mchezo wowote zaidi ya sare mbili.
Kagera wapo nafasi ya tano. Wakiwa tayari wamecheza game 9, timu hiyo ya Bukoka imefanikiwa kushinda game nne, wamepoteza mara mbili na kupata sare katika michezo miwili.
Wakiwa na pointi 13, kikosi cha Mecky kimefanikiwa kufunga magoli manne tu na kuruhusu nyavu zao mara nne hivyo kuwa na wastani wa goli 0.
‘Timu zote zimetoka kushinda katika michezo yao ya ugenini siku ya Jumatano. Simba ilishinda 2-0 vs City wakati Kagera ilipata ushindi wa goli 1-0 vs Majimaji.
MTIBWA v PRISONS
Kocha, Salum Mayanga alikuwa na nyakati nzuri msimu uliopita baada ya kuisaidia Prisons kumaliza katika nafasi ya nne kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2007/08.
Aliiongoza Prisons katika game 15 pasipo kupoteza katika uwanja wake wa nyumbani-Sokoine, Mbeya na baada ya mafanikio hayo akaamua kukubali kazi ya kuifundisha Mtibwa, timu ambayo ‘imemlea’ kwa kipindi kirefu.
Mtu aliyeshika nafasi yake pale TP, Meja mstaafu, Mingange yupo katika ‘kuti kavu’ na safari ya kutimuliwa kuwanoa maafande hao wa Jeshi la Magereza inaweza kutimia baada ya dakika 90′ za pambano hili litakalopigwa Manungu, Complex.
Mtibwa ilipoteza mechi yake ya 3 msimu huu siku ya Jumatano baada ya kuchapwa 3-1 na Yanga, matokeo hayo yamewaporomosha kwa nafasi moja kutoka nafasi ya 3 hadi ya nne.
Prisons wamefanikiwa kushinda michezo miwili tu kati ya 9 waliyokwisha cheza. Wametoa sare katika game 5 na kupoteza mchezo mmoja tu.
Timu hiyo ya Mbeya imekuwa ikiangushwa na ufungaji, kwani hadi sasa wamefanikiwa kufunga magoli matatu.
Safu yao ya ulinzi imekuwa nguzo kubwa ya pointi zao 11 kwani licha ya kucheza game 9 wameruhusu nyavu zao mara mbili tu.
Idadi ya chini ya magoli ya kufungwa kwa timu zote. Mtibwa imefunga magoli 9 lakini safu yao ya ulinzi imeruhusu magoli 9 pia hivyo wana wastani wa goli 0.’
STAND v LYON
Kitendo cha Simba kushindwa kuifunga Kagera Sugar na Stand ikapata ushindi vs Lyon kitaifanya Stand kwenda kileleni mwa msimamo.
Ikiwa na alama 19 (pointi 1 nyuma ya Simba) kikosi cha Mfaransa, Patrick Liewig kinajivunia ushindi wa michezo mitano na sare nne katika game zao tisa.
Wanakutana na Lyon iliyo nafasi ya 12 na pointi zao 9. Stand iliifunga Azam FC katikati ya wiki hii wakati Lyon ilipoteza 2-0 mbele ya Mwadui FC.
Lyon imefunga magoli matano na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara kumi, wakati Stand imefunga magoli 9 na kuruhusu matatu katika lango lao.

Share on Google Plus

About omary omary

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment