KULIKUWA na ulazima gani wa ligi kuu Tanzania Bara kuendelea Disemba 17 na 18? Najiuliza ni kwanini Shirikisho la Soka nchini-TFF linashindwa kutambua na kupanga muda sahihi wa usajili wa dirisha dogo? Je, TFF haitambui uwepo wa michuano ya Mapinduzi Cup?
Wakati Yanga SC ilipoenda kileleni mwa msimamo wa ligi kuu kwa mara ya kwanza msimu huu siku ya Jumamosi, rekodi ya Ndanda FC vs Simba katika michezo mitano ya nyuma ilikuwa na taarifa upande wa mabingwa watetezi-taarifa inayowaambia kikosi cha Mzambia, George Lwandamina kitakuwa kileleni kwa masaa yasiyozidi 24 tu.
Na baada ya dakika 90′ za pambano la Jumapili kumalizika katika uwanja wa Nangwanda, Ndanda 0-2 Simba, kikosi cha Mcameroon, Joseph Omog kikarejea kileleni.
Wakati vigogo hao wakishinda, timu iliyomaliza nafasi ya pili mara tatu na kutwaa ubingwa mara moja, Azam FC wameshindwa kufunga hata goli dhidi ya timu iliyoruhusu magoli 15 katika michezo 15 ya mzunguko wa kwanza-African Lyon.
Pointi 12 nyuma ya vinara Simba na pointi 10 nyuma ya mabingwa watetezi Yanga, Azam nawaondoa rasmi katika mbio za taji.
Ratiba yao ijayo ni ngumu kutokana na kushindwa kufunga sana magoli. Disemba 31 watakuwa Songea kucheza na Majimaji FC. Januari 7 watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons-timu yenye ukuta mgumu lakini wanaweza kufunga hata goli moja na kulilinda.
Kama ‘mwarobaini’ wa kutatua matatizo ya ufungaji yatashindwa kutibu, Mhispaniola, Zeben Hernandez atakuwa na kibarua kizito dhidi ya timu nyingine iliyowasaini wachezaji wengi wapya katika dirisha dogo-Mbeya City FC mechi inayoonekana katika ratiba itachezwa Januari 14.
Niliuliza kuna maana gani mzunguko wa pili wakati huohuo kuna timu zitaenda kucheza michuano ya wiki mbili-Mapinduzi Cup huko visiwani Zanzibar. Michuano hiyo katika miaka ya karibuni imekuwa ikifanyika kila mwaka kuanzia mwishoni mwa mwezi Disemba hadi Januari 13.
Yanga, Simba, Azam FC, Mtibwa Sugar (mwaka huu Mtibwa hawajaalikwa) zimekuwa zikicheza michuano hiyo na ikumbukwe, Yanga walipojitoa katika michuano hiyo miaka miwili iliyopita-hata serikali ‘iliwakemea’ kwa sauti kali, na walikuja kuomba msahama ambao uliambatana na kiasi fulani cha pesa.
Wakasamehewa na hakuna timu iliyoyapuuza tena mashindano hayo maalum ya kusherekea kumbukumbu ya Mapinduzi ya Zanzibar, Februari 12, 1964. Sasa mbona katika ratiba ya Yanga inaonyesha mabingwa hao watetezi wanapaswa kucheza na African Lyon, Januari Mosi, 2017.
Januari 7 wanapaswa kucheza na Ndanda FC, kisha Majimaji FC Januari 14.
Si Azam FC na Yanga tu, hata upande wa Simba ratiba yao ijayo inaonesha watakuwa wenyeji wa JKT Ruvu Jumamosi Disemba 24, kisha watacheza na Ruvu Shooting Januari 8, 2017 halafu wataenda kucheza na Mtibwa Sugar siku ya Januari 15.
Tarehe za michezo ya timu hizi tatu zinaingiliana na ratiba ya michuano ya Mapinduzi. Kwa namna ligi ilivyo, mbio za taji msimu huu zitawahusu ‘Kurwa na Dotto,’ lakini mpangilio wa ratiba ni mbaya na unapunguza msisimko halisi za mbio za taji. Baada ya michezo ya mzunguko wa 16 kuchezwa Disemba 17 na 18, michezo ya mzunguko wa 17 itachezwa Disemba 23, 24 na 26.
Kutokana na uwepo wa michuano ya Mapinduzi hapo Yanga, Simba na Azam FC hawatacheza VPL. TFF ingerefusha usajili wa dirisha dogo, angalau ufike hadi Januari Mosi.
Wakati mwingine mbio za ubingwa kati ya timu mbili zenye mwelekeo wa kushinda taji hupendezeshwa kwa aina ya ratiba yenye mtiririko mzuri.mfano, michezoya raundi ya 16 imechezwa Disemba 17 na 18, baada ya hapo timu zitarudi viwanjani Disemba 31 na Januari 1,2017. Karibia wiki mbili.
Simba,Yanga na Azam FC zitaenda Zanzibar, hivyo kuna michezo ya ligi haitochezwa. Ligi inaweza kuendelea kusimama mara baada ya michezo ya mzunguko wa kwanza, lakini wakati sahihi kuanza mzunguko wa pili ni kuanza baada ya kumalizika kwa Mapinduzi Cup. Ilikuepuka kutosimama simama.
0 comments:
Post a Comment